Thursday 18 August 2016

NGUVA>>>SOMA TABIA ZA NGUVA



Mnyama aina ya Nguva ambaye watu wamekuwa wakimwelezea kwa namna tofautitofauti, yuko hatarini kutoweka endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa
Watu wengi hawajui uhalisi wa mnyama huo kwani baadhi ya watu wamekuwa wakisema ni upande mmoja samaki na mwingine mwanamke. 

Makumbusho ya taifa ambayo ndiyo ina dhamana ya kuhifadhi mambo ya kale imeweka wazi ukweli kuhusu nguva na maisha yake. Mkurugenzi wa Makumbusho hayo, Bw. Paul Msemwa, anasema mnyama huyo mambo mengi ambayo yamekuwa yakizungumzwa kuhusu mnyama huyo si ya kweli. 

Anasema nguva ni mnyama anayezaa na kunyonyesha kama walivyo wanyama wengine. Anasema wakati akinyonyesha husimama na kukumbatia mtoto wake hali inayoweza kumfanya mtu aliyemuona kudhani kuwa ni mtu. 

Anaeleza kuwa watu wengi hawajui ukweli kuhusu nguva na baadhi wamekuwa wakisema kuwa ni nusu mtu. ``Kuna watu wanapotosha wanasema nguva ni nusu mtu kwa maana kuwa chini ni samaki na juu ni mtu lakini si kweli,`` anasema. 

Anasema muda mrefu mnyama huyo hukaa baharini na kwamba anapenda mazingira mazuri na tulivu. Dk. Msemwa anasema mnyama huyo huzaa kila baada ya miaka mitatu au saba na huzaa mtoto mmoja pekee. Mtoto wa mnyama huyo anapozaliwa huwa na kati ya kilo 153 hadi 200, wakati nguva mkubwa huwa na kati ya kilo 400 hadi 1, 000. Dk. Msemwa anataja maeneo ambayo wanyama hao hupatikana kuwa ni Somanga karibu na Rufiji, Kilwa, Mafia, Moa Mombasa, Tanga na Bagamoyo. 

Anasema endapo mazingira ya bahari yataendelea kuchafuka kuna uwezekano wa kiumbe hicho kutoweka. Alisema kwa kawaida nguva hupenda maeneo tulivu na yasiyo na vitisho. 

``Huu uvuvi haramu wa mabomu na baruti utasababisha wanyama hawa kutoweka kabisa kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa,`` anasema. Anasema mnyama huyo hupendelea zaidi kula majani yaliyo chini ya bahari maarufu kama mwani. 

Nguva ana rangi ya kijivu na umbo la mwili wake ni nyofu na uso wa umbo la nguruwe. 

Awapo katika maji hutoa kichwa chake juu ya maji kuvuta hewa kwa kutumia mashimo mawili ya pua yaliyopo upande wa juu wa kichwa chake. Dk. Msemwa anasema nguva jike ana chuchu kifuani na anaponyonyesha mwanaye husimama kwa kutumia mkia wake chini na kumkumbatia mwanaye kama binadamu. Aidha, anasema tayari wameanza kuwaelimisha wavuvi kuhusu mnyama huyo ili wamwonapo wasimvue. 

Anasema kuna wakati wavuvi walikuwa wakiwavua na kuwala kwa kuwa nyama yao ni tamu zaidi ya ile ya ng�ombe. Anasema kutokana na mazingira kuharibiwa, hivi sasa mnyama huyo ameanza kutoweka sehemu ambazo alikuwa akionekana. 


``Alikuwa akionekana Dar es Salaam, Kimbiji, Buyuni, lakini sasa haonekani tena na hali hii inatokana na usumbufu wa wavuvi na mazingira ya bahari kuchafuliwa,`` anasema. 

Anasema mnyama huyo ana aibu na anapogundua kuwa maeneo alipo kuna binadamu huhama na kwenda mbali zaidi. Dk. Msemwa anasema vifo vya nguva vimekuwa vikitokana na ajali za bahati mbaya mfano kunaswa kwenye vyombo vya kuvulia kama vile jarife, mishipi na kuongezeka kwa shughuli za uvuvi. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Viumbe katika makumbusho hayo, Bi. Adelaide Sailema alisema wameanza kuelimisha wavuvi ili wanapowaona wanyama hao wasiwavue. Anasema kuna umuhimu wa kuweka maeneo tengefu kwa ajili ya kuwahifadhi wanyama hao. 

``Tumeishauri serikali itenge maeneo ambayo mnyama huyo anapatikana ili wasitoweke,`` anasema. Anafafanua kuwa mtawanyiko wa nguva upo zaidi maeneo ya Somanga, Kilwa, delta ya Rufiji, Mohoro na Mafia kuanzia miaka ya 1960. 

Anasema nguva amekuwa akionekana mara nyingi zaidi miaka ya 1950 sehemu za Kilwa Kivinje miaka ya 1960 sehemu za Mkwaja na Matapata miaka ya 1970 sehemu za Kilwa kisiwani, Kilwa Masoko na kaole miaka ya 1980 sehemu za Somanga, Pombwe na Olelo miaka ya 1990 sehemu za Masoko Pwani na miaka ya 2000 sehemu za Somanga, Utigi Ngolwe, Pombwe na Mbonde. 

Sehemu zingine zilizoripotiwa kuwa na nguva ni Lamu, pangani, Tanga, Buyuni, Kimbiji, Unguja, Pemba, Mafia na Kisiju. Dk. Msemwa anasema nguva anahitaji kuhifadhiwa kwa kutovuliwa kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho. Wakati huo huo, anasema ukumbi wa kudumu wa viumbe (biolojia) ni kati ya kumbi nne za kudumu zilizopo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni. 

Anasema ukumbi huo ulianzishwa rasmi mwaka 1980 baada ya kumbi nyingine kuwepo ambazo ni ukumbi wa chimbuko la Mwanadamu, ukumbi wa historia ya Tanzania na ukumbi wa mila na desturi za Mtanzania. Anasema ukumbi wa viumbe ulipoanzishwa ulilenga zaidi maonyesho ya viumbe bahari na mara nyingi ulijulikana ukumbi wa viumbe bahari (Marine Biology Gallery). 

Anasema moja ya maonyesho yaliyopo katika ukumbi huo ni maonyesho ya mnyama Nguva ambaye kwa mara nyingi amekuwa akiamisha maswali na majibu ya aina mbalimbali kutoka katika jamii kama ni nusu samaki na nusu mwanamke. 

Anaeleza kuwa kutokana na mahitaji mbalimbali ya jamii yaliyojitokeza, ilionekana kuwa ni sahihi kuwa na viumbe kutoka katika mifumo ikolojia mbalimbali ili kuweza kukidhi haja. Anasema kwa sasa mikusanyo iliyopo imegawanyika katika sehemu kuu tatu kutokana na mifumo ikolojia ilikotoka mikusanyo hiyo. 

Anatoa mfano wa mfumo ikolojia wa bahari Wenye wanyama wanyonyeshao, samaki, kamba kochi, kasapweza, miamba ya matumbawe, majongoo bahari, konokono na kaa.

0 comments:

Post a Comment

Bonyeza hapa ushinde pesa