Sunday 21 August 2016

Kama unataka kumuoa Johari inakuhusu!


STAA wa kitambo kwenye filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’ amesema baada ya kukaa singo kwa muda mrefu, sasa yupo tayari kuingia kwenye ndoa wakati wowote.
Akizungumza na Swaggaz, Johari amesema anatamani sasa naye aingie kwenye ndoa kwa kuwa umri wake unamruhusu kufanya hivyo.
“Mimi ni mwanamke kamili, ni mtu mzima. Nimeshakuwa sasa, kwahiyo kiukweli nina kiu ya mume. Mungu akinipa mume bora, nitaolewa. Sitaki kuzungumzia sana mambo yaliyopita, lakini muhimu kwa sasa ni mume,” anasema Johari.
Kuhusu sifa za mwanaume anayependa awe mumewe, Johari alisema: “Napenda mwanaume mwenye upendo wa dhati   kwangu na awe mtafutaji, pia aheshimu kazi yangu.
“Historia yangu ya mapenzi imenifundisha mengi, najielewa na kujitambua vizuri. Kuna tofauti kubwa sana kati ya Johari wa zamani na wa sasa. Kwanza nimekomaa kiakili, nimekutana na vitu vingi na nimejua maisha ni nini. Nipo tayari kufanya maisha na mwanaume serious.”
Hata hivyo, Johari anasema kuwa ikitokea mwanaume wa kumuoa akichelewa sana, atafikia uamuzi wa kuzaa, kwani ni kati ya ndoto zake za muda mrefu.
“Hakuna mwanamke ambaye hapendi kuitwa mama. Hata mimi natamani, nitajisikia fahari sana siku moja nikiitwa  mama. Ingawa siyo vyema kuzaa nje ya ndoa, lakini ikitokea mwanaume wa kunioa anachelewa nitachukua uamuzi huo mgumu,” anasema Johari.
UJIO MPYA
Johari ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya RJ ya jijini Dar es Salaam akiwa na mkurugenzi mwenza, Vincent Kigosi ‘Ray’ amesema kwa muda mrefu alikaa kimya kisanii, lakini sasa amerejea upya.
“Nimeamua kuanza na nyumbani kwetu Mwanza. Nina movie inaitwa Dosari ambayo nimecheza na wasanii wa Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwasapoti. Ni filamu ya Kampuni ya Freedom Fighter Film inayomilikiwa na Freedom (Edward Kumaliga),” anasema.
Anasema filamu hiyo ambayo itasambazwa na Kampuni ya Steps Entertainment ya jijini Dar es Salaam, imechezwa na wasanii wa Kanda ya Ziwa wakiwemo Freedom na Andrew Ngonyani ‘Braza K’ anayeshiriki kwenye mchezo wa Futuhi unaorushwa na Star TV.
“Baada ya kazi hii, kuna mzigo mwingine utaingia sokoni kupitia kampuni yetu ya RJ. Wadau watulie, wasubiri kazi za nguvu kutoka kwangu. Nimepania kurudisha ushindani  uliokuwepo zamani,” anasema Johari.
Lakini hata hivyo, Johari alieleza malalamiko yake kuhusu soko la filamu lilivyoshuka nchini tofauti na zamani ambapo alisema sababu kubwa inayosababisha hali hiyo ni kuwa na wasambazaji wengi wasiokuwa na uwezo na kazi hiyo.
“Soko la filamu siyo zuri sana kutokana na usambazaji pamoja na wimbi la watengenezaji wengi waliojitokeza pasipokuwa na uwezo na vigezo. Kingine naweza kusema ni uhaba wa wasambazaji wenye uwezo na kazi hiyo,” anasema Johari.

0 comments:

Post a Comment

Bonyeza hapa ushinde pesa